Feb 14, 2012

TATHMINI YA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE MWAKA 2011/ Wilaya ya Tunduru

WILAYA YA TUNDURU, MKOA WA RUVUMA

Matokeo ya kidato cha nne yalitangazwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (NECTA), Dk. Joyce Ndalichako siku ya tarehe 7/02/2012. Matokeo hayo yanaonyesha kuwa asilimia 54 ya wanafunzi 426,314 waliofanya mtihani huo wamefaulu, yaani wamepata daraja la I, II, III na IV; huku asilimia 46 ya wanafunzi hao wakipata daraja la 0. Lakini katika ya hao wanafunzi 426,314 waliofanya mtihani, ni asilimia 10 tu ndio walifaulu kwa kiwango cha daraja la I mpaka III na hivyo kuwa na sifa za kuendelea na kidato cha tano.

Lengo la tathmini hii sio kuangalia ufaulu wa wanafunzi wa nchi nzima; bali kuangalia kiwango cha ufaulu wa wanafunzi katika wilaya ya Tunduru ili kuisaidia Tunduru Development Forum (TuDeFo) kujadili na kutathmini namna ya kusaidia kuboresha elimu katika wilaya ya Tunduru. Katika tathmini yangu nitatazama matokeo ya shule 14 kati ya zilizopo katika wilaya hiyo. Tathmini yangu itaziangalia shule zifuatazo; Tunduru Sekondari, Mataka, Frankweston, Nandembo, Namasakata, Marumba, Semeni, Mbesa, Matemanga, Lukumbule, Nakapanya,Masonya, Nalasi na Kiuma.

Kiujumla, takwimu zinaonyesha kuwa wanafunzi 1,029 walifanya mitihani hiyo katika shule hizo 14 nlizozitaja. Kati ya hao 1,029, mwanafunzi mmoja (kutoka Nandembo sekondari) amepata daraja la I, wanafunzi 5 wamepata daraja la 2, wanafunzi 49 wamepata daraja la 3, wanafunzi 528 wamepata daraja la 4 na wanafunzi 446 wamepata 0.

Kwa kuangalia takwimu hizo, wilaya ya Tunduru imefanya vibaya katika mitihani hiyo kwani ni wanafunzi 583 (asilimia 57) ya wanafunzi 1,029 waliofanya mitihani hiyo ndio waliofaulu, huku wanafunzi 446 (asilimia 43) wakifeli. Kati ya hao, ni wanafunzi 55 tu kati ya 1,029 (asilimia 5) ambao wana sifa za kuendelea na kidato cha 5 kwa maana kuwa wamepata daraja la I mpaka la III. Wanafunzi 974 kati ya 1,029 (asilimia 95) walipata daraja la IV na O na hivyo kukosa sifa za kuendelea na kidato cha 5. Kwa takwimu hizo tu, tunaona kuwa hali ya elimu kwa wilaya yetu bado ni mbaya sana.

Tathmini inaonesha pia kuwa kati ya wanafunzi 55 waliopata daraja la I mpaka la III, ni wanafunzi 20 tu ndio wenye sifa za kuchaguliwa shule za serikali kwa ajili ya kidato cha 5 kwa sababu wamepata angalau alama ya C katika masomo yote ya michepuo waliyochagua. Wanafunzi 35 wanaweza wasichaguliwe kuendelea na kidato cha 5 kwa kukosa sifa hiyo. Hata hivyo kwa wanafunzi wenye uwezo wa kifedha kati ya hao 35 wanaweza kuendelea na kidato cha 5 katika shule za binafsi bila kuhitaji kurudia mitihani yao.

Tathmini pia inaonyesha kuwa wanafunzi wengi wamefaulu masomo ya sanaa ‘Arts’ na kufeli sana masomo ya sayansi hasa Hesabu, ukiondoa Kiuma ambao wamefaulu sana masomo ya sayansi na kufeli masomo ya sanaa. Hata hivyo, matokeo hayo yameonesha kuwa wanafunzi wengi wameshindwa ‘kubalance’ ufaulu katika masomo hayo kwani wale waliofaulu masomo masomo ya sanaa hawakufanya hivyo katika masomo yote ya sanaa na wale waliofaulu masomo ya sayansi hawakufanya hivyo katika masomo yote ya sayansi pia.

Kutokana na takwimu hizo, yafuatayo inabidi yafanyike ili kuinusuru wilaya ya Tunduru kielimu. Kwanza, kuboresha utoaji wa elimu katika shule za msingi ili kupata wanafunzi wazuri wanaoingia shule za sekondari. Uboreshaji huo uende sambamba na kuweka misingi mizuri katika masomo ya Hisabati na Kiingereza kwa sababu ndiyo yanayosaidia sana katika shule za sekondari. Hili lifanyike kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wa elimu katika wilaya, yaani wazazi/walezi wa wanafunzi, maafisa elimu wa wilaya na kata, wakaguzi wa elimu na jamii nzima ili kuhakikisha kuwa walimu wanatoa elimu bora katika shule hizo ambayo itawasaidia wanafunzi katika shule za sekondari.

Pili, Kuboresha mazingira katika shule za sekondari ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za walimu za kutosha ili walimu wapya wasikimbie kufanya kazi katika shule hizo. Shule nyingi hazina walimu wa kutosha kutokana na walimu wengi kukimbia kufanya kazi katika shule hizo. Hii inatokana na shule kutokua na majengo ya kutosha kwa walimu kuishi hasa katika maeneo ya vijijini, na hivyo kusababisha wanafunzi kukaa muda mrefu bila walimu wa masomo husika.

Tatu, kutoa motisha kama pesa na/au samani za ndani kwa walimu wapya ili kuwatia moyo wa kubaki kufundisha katika wilaya yetu. Walimu wengi wapya wanakua na matarajio makubwa pindi wanapopata kazi kwa mara ya kwanza. Matarajio yao yanaposhindikana huanza kufikiria namna ya kuondoka maeneo hayo na kutafuta maisha sehemu nyingine ili kutimiza matarajio yao. Motisha hizo zitasaidia kuona tunawajali na hivyo kujitolea kwa moyo wote kufundisha katika maeneo hayo bila kukimbia.

Nne, kuanzisha utaratibu wa kusomesha wanafunzi wa ualimu (wazawa) ambao watakapomaliza watalazimika kurudi kufundisha katika wilaya ya Tunduru. Hii itapunguza gharama kubwa ya kuondokewa na walimu mara kwa mara na hivyo kupunguza tatizo la wanafunzi kukaa bila walimu kwa muda mrefu. Walimu wazawa watakua na uchungu na jamii ya Tunduru na hivyo kufundisha kwa uchungu zaidi kuliko walimu wageni. Fedha za kusomesha wanafunzi hao zitapatikana kwa michango ya hiyari ya watu/taasisi mbali mbali ikiwemo mfuko wa jimbo wa mbunge.

Tano, kuanzisha mijadala endelevu (makongamano, matamasha, mashindano katika masomo n.k) katika wilaya yenye lengo la kuelimisha wanafunzi na jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa elimu kwa maendeleo ya wilaya. Mijadala hiyo itahusisha wadau mbalimbali katika elimu na itawakusanya wanafunzi wengi katika kanda tofauti ili kuamsha ari ya kupenda elimu miongoni mwa wanafunzi na wazazi.

Sita, Kutoa zawadi kwa wale wote waliofaulu vizuri mitihani ya kidato cha nne na kuwasaidia wale waliopata daraja la 3 lakini hawana sifa za kuchaguliwa shule za serikali ili waweze kuendelea na kidato cha 5 katika shule binafsi. Ni vizuri katika hili, tukasaidia hao vijana ili badae wasomee ualimu na kuendelea kufundisha katika shule ambazo zipo ndani ya wilaya yetu.

Naomba niishie hapo ili niwape nanyi nafasi ya kujadili kwa maslahi ya wilaya yetu huku tukiweka kando aina yoyote ya siasa katika hili.

Created By Stanley Mark Shirima Member wa TuDeFo
Dar es Salaam
Silvanus

No comments: