Dec 20, 2011

Flood in Dar es salaam


Huyu mbunge ni mfano wa kuigwa.. Jiji la Dar es Salaam lina wabunge wasiopungua watano.. Lakini hakuna hata mmoja aliyekunbuka kusaidia kazi uokoaji katika maafa ya Mafuriko, ila Mbunge huyu wa Mafia Mh. Abdulkarim Shah, aliye jitolea Boti na yeye mwenyewe kuthubutu kuingia kazini kama munavyo muona kwenye picha... Wabunge wetu acheni usharobaro.




JIJI la Dar es Salaam na vitongaji vyake, limekumbwa na maafa ya vifo vya watu watano akiwamo mmoja aliyepigwa na radi, uharibifu wa miundombinu huku mamia ya watu wakikosa makazi, kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia jana.Mvua hizo zilisababisha tatizo kubwa la usafiri kutokana na barabara kujaa maji, kuezua nyumba na kuua watu watano na kuacha maelfu ya wakazi wa jiji hilo bila makazi baada ya nyumba zao kuezuliwa mapaa.

Mvua hiyo ilianza kunyesha mnamo saa 9:00 alfajiri ikiambatana na radi na ngurumo nzito na kusababisha kukatika mara kwa mara kwa umeme katika baadhi ya maeneo ya jiji hilo ambalo ni kitovu kikuu cha biashara na uchumi kwa nchi.

Waandishi wa gazeti hili waliotawanyika sehemu mbalimbali za jiji hilo, walishuhudia maiti za watu wawili waliozolewa na maji maeneo ya Sinza na Msewe.

Wakati maiti moja ikitambuliwa kwa jina la Ibrahimu Lusama (60), maiti nyingine ambayo ilipatikana katika Bonde la Mto Ng'ombe bado haijatambuliwa.

Hata hivyo, moja ya maiti hao alisemekana anatoka eneo la Msewe na aliokotwa eneo la Sinza Iteba, takriban umbali wa kilometa tano. Madaraja ya Msewe na Sinza Iteba yalivunjika na kusababisha usumbufu mkubwa kwa abiria wanaotumia madaraja hayo.

Madaraja mengine yaliyovunjika ni pamoja na daraja la Msewe na la mto wa Ng’ombe, huku magari yaliyokuwa yakienda Mwananyamala, Mikocheni yakitokea Ubungo yakilazimika kusitisha safari zake baada ya kujaa maji.

Baadhi ya maeneo ya jiji hasa Kigogo, Tandale, Mabibo na Tabata yalikumbwa na kadhia ya maji kujaa kwenye makazi yao na kusababisha usumbufu ambao ulionekana kutishia usalama wa mali na maisha.

Wazee walikuwa wakihangaika huku na kule kutafuta sehemu za kujisitiri, lakini vijana na watoto walionekana wakicheza kwenye mvua bila kujali mustakabali wao.



Wafanyabiashara wa vyakula vya jumla na rejareja katika baadhi ya maeneo waliamka na kukuta sehemu kubwa ya bidhaa zao zimeharibika huku meza na vyombo vya mama lishe, vikionekana kuelea barabarani baada ya kusombwa na maji.

Sinza
Mawasiliano ya Sinza na Tandale yalikatika baada ya daraja kusombwa na maji huku maiti ya mtu aliyeonekana kuwa mzee wa makamo ukikutwa umekwama kwenye kingo za daraja, kabla ya kuokolewa na wasamaria wema.

Mmoja wa wamiliki wa zahanati moja iliyoko Kigogo Darajani ambaye jina lake halikufahamika mara moja, alisema amepata hasara baada ya maji kuingia ndani na kuharibu vifaa mbalimbali vya hospitali zikiwamo dawa.

"Angalia, nimepata hasara sana. Mpaka sasa wasaidizi wangu wanafanya kazi ya kuzoa maji na kusafisha vitanda na baadhi ya vifaa, vingine havifai," alisema mmiliki huyo ambaye hakuwa tayari kutaja jina.

Katibu wa CCM tawi la Kigogo Wakereketwa, Charles Gumbo alisema kulikuwa na taarifa za watoto ambao hakuwataja idadi kufariki, baada ya mama yao kuwapandisha juu ya kabati kwa lengo la kuwaokoa.

Hata hivyo, kabati hilo na nyumba walimokuwa ikiishi familia hiyo vilisombwa na maji huku mama wa watoto hao akikimbia kutafuta jia ya kujiokoa.

"Hapa tunachambua mboga kutayarisha chakula cha mchana, lakini hatujui usiku itakuwaje...mvua zenyewe ndiyo kama hizi," alisema Joyce Meshack huku akionyesha kukata tamaa.

Msimbazi na hosipitalini
Mwananchi pia ilishuhudia watu kadhaa wakiwa wanaopolewa katika daraja la Mto Msimbazi, baada ya kuzolewa na maji na kukimbilia kwenye miti ya mpapai. Kazi hiyo ilifanywa na Kikosi cha Uokoji cha Polisi.

Helkopta za Polisi na Jeshi la Wananchi (JWTZ) zilionekana angani zikiwa zinafanya doria katika maeneo yalioyodhurika kutokana na mafuriko hayo.

Katika Hospitali ya Manispaa ya Ilala (Amana), watu kumi walifikishwa kwa ajili ya matibabu baada ya kuopolewa kwenye maji maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo.

Mganga anayeshughulikia maafa katika hospitali hiyo, Christopher Mzava alisema majeruhi hao waliofikishwa hospitalini hapo kwa nyakati tofauti kuanzia saa 12:00 asubuhi jana.

Katika Hospitali ya Temeke mtu aitwae Gate Mseti ameokotwa baada ya kupigwa na radi huku akiwa na mtoto Thobias Rashid (6) ambaye amejeruhiwa.

Muuguzi wa zamu wa hospitali hiyo, Senzota Khalifa alisema wamepokea watu wawili mmoja akiwa amekufa huku mtoto aliyekuwa amejeruhiwa akiruhusiwa na kuongeza kwamba, maiti hiyo ilipelekwa hospitalini hapo na wasamaria wema wakiongozwa na polisi aliyejulikana kwa jina la James. 

Katika Hospitali ya Mwananyamala, kulipelekwa maiti watatu na majeruhi wawili na mmoja kati yao alipelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.

Katibu wa Afya wa Hospitali hiyo, Edwin Disakara aliwataja marehemu hao kuwa ni Ibrahim Lusama wa Ubungo Maji (60), Vivian Maximilan wa Mburahati (13) na mtoto mmoja mwenye umri wa miezi kadhaa aliyeokotwa kwenye tope.

Alisema majeruhi ni Hawa Yusuf mkazi wa Tandale na Tatu Juma ambaye baadaye alipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Polisi na Serikali ya mkoa
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Suleiman Kova alithibitisha vifo vya watu watatu akieleza kuwa vyote vimetokana na mvua hizo.
Alitaja waliofariki kuwa ni mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Jackline (33), ambaye ni Mkazi wa Kitunda. Alisema mwanamke huyo alikufa baada ya kupigwa na radi akiwa amempakata mwanaye, lakini mtoto alipona.
Kwa mujibu wa Kova, wengine waliofariki dunia ni Maganga Said (8) Mwanafunzi na Mkazi wa Kiwalani ambaye alikanyaga waya wa umeme uliokuwa umeanguka chini na Ibrahimu Lusama (60) aliyefariki baada ya kuzolewa na maji katika daraja la Msewe.
Kova aliwataka wakazi wanaoishi mabondeni kuondoka mara moja kupisha mvua hizo ambazo Mamlaka za Hali ya Hewa imesema zitaendelea kunyesha mfululizo kwa siku kadhaa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick alithibitisha vifo hivyo na kueleza kuwa maiti ya mtu aliyetambuliwa kwa jina la Lusama, alizolewa na maji kutoka daraja la Msewe mpaka Mto wa Ng’ombe.

"Hali ni mbaya sana kwa jiji la Dar es salaam, kwani watu wamepoteza maisha na makazi yao pamoja na mali," alisema Sadick na kuongeza:

“Tulishatangaza watu wahame mabondeni jamani, lakini bado wanaendelea kukaa tu huko na haya ndio matatizo yenyewe,”alisema

Awali Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya za Ilala na Temeke, alisema katika wilaya zote tatu, wilaya ambayo imeathirika zaidi ni Kinondoni ambako kumetokea maafa.

“Kinondoni ndiko hasa kulikotokea maafa makubwa, wilaya nyingine ni salama,”alisema Rugimbana.



Utabiri wa TMA
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mvua hizo zitaendelea kunyesha mfululizo kwa siku mbili zaidi.



Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Agness Kijazi alisema jana kuwa, mvua hizo zimesababishwa na upepo kutoka nchi za Kongo na Msumbiji unaopeleka joto katika Bahari ya Hindi.



Alisema mvua hizo zitaendelea kunyesha kutokana na wingu zito lililotanda katika maeneo ya Pwani ya Kaskazini ya mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro,Tanga na visiwa vya Unguja na Pemba. 
Maeneo mengine ni mikoa ya Singida, Dodoma, Mbeya na Iringa.
"Wingu hilo limesababisha mvua kubwa ambayo inaendelea kunyesha katika baadhi ya maeneo hayo kwa hali hiyo inatarajiwa kuendelea kwa muda wa siku mbli zijazo"alisema Kijazi.





Rescuers wade in the floodwater to save a person who had sought refuge on a tree at the Kigogo valley in Dar es Salaam yesterday morning.  

Flood result

People suffered alot





No comments: